Rais Samia ameagiza Mzee Hashimu Msuya na Mke wake ambao ni Wazazi wa Watoto wanne waliofariki watibiwe VIP
Rais Samia ameagiza Mzee Hashimu Msuya na Mke wake ambao ni Wazazi wa Watoto wanne waliofariki usiku wa kuamkia August 03,2023 baada ya gari lao (Prado) kugongana uso kwa uso na Lori Mkoani Pwani, watibiwe kwa hadhi maalum (VIP Treatment) kwenye Hospitali za Muhimbili, JKCI na wasisumbuliwe kimatibabu kwenye Hospitali yoyote nchini.
Akiongea leo wakati wa Ibada ya kuuga miili ya Watoto watatu, RC wa Dar es salaam Albert Chalamila amesema “”Mh.Rais wakati ananituma hapa alisema nimesoma kwenye mtandao Watoto wale walikuwa wanawalea Wazazi wao, walikuwa wanawapeleka Hospitali na akaniambia niongee na Prof.Janabi wa pale Muhimbili, niongee na Dkt.Kisenge wa JKCI kwamba Wazazi hawa wapate VIP treatment watakapokwenda Hospitali pale”
“Na jukumu hilo akaniambia waambie na Wakuu wa Mikoa wengine wote mahali popote watakapokuwepo Wazazi hawa wasiwe na mnyororo mpana wa kusumbuka mwisho wataanza kuwakumbuka Watoto wao kama sisi tutaendelea kutokuwa faraja yao”
Miili ya Siah Hashimu Msuya (53), Diana Sukulu Mageta (47) na Dkt. Norah Msuya Mumburi (45), imeagwa leo Dar es salaam na mwili wa Kaka yao (Dereva wa Prado) ambaye walipata nae ajali hiyo, Neech Hashim Msuya ambaye alikuwa Mfanyakazi wa Benki ya ABSA tayari umeshazikwa Jumapili katika Kijiji cha Msangeni Ugweno Wilayani Mwanga, Kilimanjaro.