Kwa Ushauri na Tiba Juu ya Tatizo lolote linalokusumbua TUWASILIANE HAPA.

Bofya hapa
Utafiti

Kujifungulia kwenye Maji kwapunguza vifo na maumivu ya uchungu

Kujifungulia kwenye Maji kwapunguza vifo na maumivu ya uchungu

Safari ya kujifungua huwa tofauti kwa kila mwanawake, na husheheni uchungu na maumivu kwa viwango tofauti.

Wakati mwingine hali inaweza kuwa mbaya na kusababisha kifo cha mama au mtoto.

Lakini wataalamu wamekuwa wakijaribu mbinu za kupunguza vifo na pia maumivu ya uchungu, na mojawapo ya mapendekezo ni kujifungulia kwenye maji.

Hatua hii imekuwa ikifanyika katika nchi tofauti, ikiwemo Tanzania ambapo tunamuaangazia mkunga Agness Ndunguru ambaye amekuwa akisaidia wanawake wajawazito kujifungua kwa njia hii.

Agness Ndunguru ni mkunga mtaalamu, na amekuwa mhamasishaji mkubwa kwa wakina mama kujifungulia kwenye jakuzi na hata kutia chachu kwa wataalamu wengine kutumia njia hii ya kutoa huduma kwa wakina mama wanaotaka kujifungua.

Anasema njia ya kujifungulia kwenye maji ilianza miaka ya 1800 katika nchi mbalimbali ambapo wanawake walikuwa wanakwenda pembezoni mwa mito au Bahari, hukaa huko wakati wakiwa katika hatua za kujifungua wakiamini kuwa inapunguza maumivu na kutumia saa chache za kusubiri muda wa kujifungua.

‘’Wanasayansi walifanya utafiti wakaona kuwa ni njia yenye mafanikio kwa mama, inampa hali ya utulivu na amani na maana yake ni kuwa kile kichocheo cha kusaidia maendeleo ya kujifungua yawe vizuri kinapanda kwa hivyo hufanya njia ifunguke vizuri na mtoto atazaliwa vizuri’’, anasema mkunga Agness.

Akina mama hutumia huduma hii kujifungulia kwenye maji huku wengine huchagua kuingia kwenye maji wakiwa katika hatua za awali kisha hujifungulia nje ya jakuzi.

Mkunga Agness anasema kujifungua kwa aina hii humpunguzia maumivu lakini pia, husaidia mama kutochanika au kuondoa kwa kiasi kikubwa hatari ya mama kuchanika uke wakati wa kujifungua.

‘’ Maji yenyewe huwa yanasaidia maeneo ya uke kutochanika lakini pia mkao wa mama kwenye jakuzi husaidi mtoto kutoka vizuri bila hatari ya mama kuchanika.’’

Hufanyika katika mazingira mbalimbali, nyumbani na hospitali kutegemea na sera ya nchi husika. Nchini Tanzania huduma hii inapatikana hospitali.

Wataalamu wanasema njia hii ni salama, kwani tafiti zinaonesha kuwa mtoto abapozaliwa kwenye maji anakabiliwa na hatari ndogo ya kupata matatizo ya upumuaji ukilinganisha na anayezaliwa nje ya maji.

Kwa kuwa mtoto anaishi kwenye maji katika mji wa mimba, hivyo anapozaliwa ndani ya maji hawezi kuhangaika kutafuta hewa ya nje.

Agnes ameweza kutambulishwa hospitali mbalimbali huu ikiwa ni mwaka wake wa pili, akisema amekuwa akipata muitikio mzuri kwasababu pia wataalamu wengi wanapitia tafiti mbalimbali kuhusu huduma hii.

Ni ndoto ya mkunga huyu kuhakikisha kuwa huduma ya kujifungua ndani ya maji inasambaa nchini kote Tanzania, kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga na wanawake.

Sikuamini kama ilikuwa inawezekana

Eminata Fabian, mkazi wa Dar Es Salaam amejaaliwa watoto mapacha, alijifungua watoto hao kwenye maji , njia ambayo imekuwa ikipata umaarufu nchini Tanzania.

Bi.Eminata aligundua huduma hii kupitia mitandao ya kijamii, hasa ukurasa wa Instagram wa mkunga Agness.

‘’Nilivutiwa pale nilipoona watu wanajifungua kwa njia ya maji na pia nilijaribu kuulizia nikaambiwa kuna nafuu sana, maumivu yanapungua tofauti na njia ya kawaida. Siku ya kujifungua sikuamini, kama ujuavyo maumivu kwa kawaida huwa makali, lakini kulikuwa na tofauti maumivu ya ndani ya maji na maumivu ya njia ya kawaida.’’ Alisema Eminata.

Eminata anasema kujifungua mapacha wake kwenye jakuzi kumemjengea hali ya kujiamini na anatamani kuendelea na njia hii kwa uzao ujao.

Tracy Isaac, mama mtarajiwa, anasema njia hii alikua akiiona kwenye filamu lakini baadaye akabaini kuwa ipo nchini.

‘’Mwanzoni nilikuwa nina wasiwasi kuwa inawezekana vipi mtoto akawa ndani ya maji mara baada ya kuzaliwa na mama anavyokuwa na utulivu wakati wa kumsubiri mtoto , kwasababu sikuwahi kushuhudia mzazi akijifungua kwa njia hii’’.

Changamoto

Kazi kubwa ya watoa huduma hii ni hamasa kwa umma kwa kuwa mara nyingi jamii haiamini kuwepo kwa huduma kama hiyo.

‘’Kwa kuwa huduma hii ni mpya nchini Tanzania kuna maswali mengi kama vile mtoto akiingia kwenye maji hawezi kunywa maji?, mtoto hatakufa?, mtoto hataambukizwa, mama hataambukizwa?

‘’Nilishawahi kukutana na visa vya mtoto kukwama mabega akiwa ndani ya maji, nilimwambia tu mama abadili mkao ndani ya maji, kwani kama unataka kumsogeza mtoto unamwambia mama asogee’’. Anasema mkunga Agnes.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeanza kutoa huduma kwa wakinamama kujifungulia kwenye jakuzi, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Profesa Mohamed Janabi amesema;

‘’Hivi leo baadhi ya wakina mama wanachagua kujifungua kwa upasuaji kuepuka maumivu au sindano ya ganzi ili kupunguza maumivu, hivyo sisi kama hospitali ya Taifa tumeona kwanini tusitumie mbinu nyingine kama zile wenzetu wanazotumia’’.

‘’Mtoto akiwa ndani ya tumbo, kwenye mfuko wa uzazi, hatumii mdomo na mapafu kupumua, hutumia njia yoyote kupitia kwa mama, sasa unapojifungulia mle anakuwa bado kwenye mazingira yanayoshabihiana na alivyokuwa awali hivyo hawi katika hali ya mshtuko baada ya kuzaliwa’’ Alisema Prof Janabi.

Ni matajario ya wengi kwamba matumizi ya njia hii hupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, lakini pia changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza kwa mama na mtoto.

Agness amepata ujuzi huu kupitia mkufunzi wake Barbara Harper ambaye ni mwanzilishi wa mafunzo ya huduma ya kuzalisha wanawake kwenye maji.

Amemuwezesha Agnes kuwa chachu kwa watoa huduma wengine nchini na amefanikiwa kufundisha watu takribani 40 ambao sasa wameweza kutoa huduma hii kwa wanawake wanaojifungua.

Agness mpaka sasa amewahudumia wanawake takribani 100, walioamua kujifungulia kwenye jakuzi.

Amekuwa akiwahamasisha wanawake na kuwapa elimu kupitia ukarasa wake wa Instagram, midwifeaggie.

Mada:Via BBC

DailyStories

Karibu DailyStories Kwa Taarifa Zote Muhimu ndani na Nje. More Updates everyday Link In http://cdp.pvh.mybluehost.me  Also Follow us on Instagram @afyaclass

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.