Kwa Ushauri na Tiba Juu ya Tatizo lolote linalokusumbua TUWASILIANE HAPA.

Bofya hapa
News

Watoto Njiti kuongezeka uzito kwa haraka kutokana na Msaada wa Mariam Mwakabungu

Watoto Njiti kuongezeka uzito kwa haraka kutokana na Msaada wa Mariam Mwakabungu.

Kati ya Agosti mosi na Novemba mwaka huu, Hospitali ya Rufaa ya Amana, imehudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati au watoto ‘njiti’ 335.

Katika kipindi kama hicho mwaka jana, walihudumiwa watoto njiti 369. Kati ya idadi hiyo ya watoto, 20 walipata rufaa kutoka hospitali zingine za pembezoni.

Inaelezwa huduma zimekuwa rahisi na watoto wamekuwa wakiongezeka uzito kwa haraka ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022.

Haya yamewezekana kutokana na ajira ambayo Serikali iliitoa kwa Mariam Mwakabungu (26), Agosti mosi, ikiwa ni siku 152 tangu Julai 19, gazeti hili liliporipoti habari kuhusu Mariam aliyejitolea kukumbatia watoto njiti wanaotupwa na kutelekezwa hospitalini hapo.

Ajira hiyo ambayo haikuwapo katika mfumo wa utumishi wa umma, imegeuka faraja kwa wanawake wanaojifungua kabla ya wakati, wauguzi na madaktari kwa kupunguza idadi ya watoto wanaokaa hospitalini kwa muda mrefu.

“Niliumwa ghafla Desemba 12, mwaka huu nikaletwa hospitali usiku, madaktari walishauri mtoto atolewe kutokana na changamoto ya kiafya, walinifanyia upasuaji. Siku mbili sikuweza kwenda kumnyonyesha.

“Nilipokuja nilionyeshwa huyu dada kwamba ndiyo alimhudumia, machozi yalinitoka nakumbuka nilimuona alipotangazwa miezi kadhaa nyuma, wala sikufikiria angenisaidia siku moja,” anasema Rehema Shayo (28), aliyejifungua mtoto wake wa kwanza kabla ya wakati.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Ofisa Muuguzi mwandamizi na kiongozi wa wodi ya watoto wachanga katika hospitali ya Amana, Mary Machemba anasema uwepo wa Mariam umewezesha watoto kupatiwa huduma bila changamoto na kukua kwa haraka.

“Watoto njiti waliohudumiwa katika wodi hii Agosti mpaka Novemba 2022 walikuwa 369 na waliofika kwa rufaa ni 32 kwa ujumla hawakutoka kwa haraka wodini,” anasema.

Idadi hiyo anasema ni kati ya watoto 4,843 waliohudumiwa kuanzia Januari hadi Desemba. “Mwaka 2023 tumehudumia watoto 4,986. Waliofika kati ya Agosti na Novemba walitoka mapema ikilinganishwa na nyakati zingine ambazo hatukuwa na msaidizi,” anasema.

“Mariam amekuwa akijitahidi kuwalea watoto, huwa wanatumia maziwa ya kopo. Akifika anautambua wajibu wake, anakoroga maziwa, anawanywesha na kama akiona tatizo kwa watoto anasimama kwenye nafasi ya mama na anatoa taarifa,” alisema. Pia amekuwa akisaidia kufundisha kinamama namna sahihi ya kuhudumia watoto na usahihi wa kumweka kifuani ili kuwezesha uzito kuongezeka haraka.

Machemba anashauri msaada wa Mariam utumike pia katika hospitali zingine. “Ninavyoamini, katika hospitali hizi kubwa zote watoto kama hawa hawakosekani, ambao mama zao wana hali mbaya au bahati mbaya wamefariki. Wapo wanaookotwa pia.”Anasema kwa kuwa idadi ya wauguzi ni ndogo na wanatakiwa watunze watoto mbadala wa mama, kuna nyakati wanakosa namna ya kuhudumiwa kwa uhakika kwa sababu muuguzi huzidiwa wakati akilisha watoto.

“Ninashauri, ili kuwa na msaada mzuri na wauguzi wajielekeze zaidi kwenye kazi zao za kutibu watoto, tupate watu kama hawa kwenye kila hospitali kubwa, ili watoe msaada wa matunzo kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine mama zao hawapo au hawawezi kuwahudumia,” alisema.

“Tuna watoto 75 humu ndani wauguzi wanaokuwa zamu ni wanne, hivyo wanatakiwa wawatunze wagonjwa, watunze wale ambao si wagonjwa.”

“Uwepo wa watu kama mimi katika hospitali nyingine, kutasaidia kurahisisha malezi kwao kwa kuwapatia huduma kwa wakati, mama zao wakiwa katika matibabu tofauti na kutegemea wauguzi pakee ambao majukumu yao ni mengi huleta changamoto kwa makuzi yao,” anasema Mariam.

Katika miezi mitano ya kazi, Mariam anasema amejifunza mambo mengi na anaendelea kujifunza akishirikiana na wauguzi.

“Matamanio yangu nifikie hatua ya kuwatibu pia, kwa sasa ninaangalia tu siruhusiwi kufanya mpaka nitakapopata mafunzo rasmi,” anasema Mariam ambaye Desemba mwaka huu alitunukiwa tuzo na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kutambua mchango wake.

Mariam anasema ataanza masomo ya sekondari mwakani pamoja na elimu aliyoahidiwa na British School.

Dr.Ombeni Mkumbwa

Ushauri|Tiba|CheckIn ContactUs; +255758286584 or INBOX. For More Healthtips everyday Link In http://cdp.pvh.mybluehost.me Also Follow us on Instagram @afyaclass