Kwa Ushauri na Tiba Juu ya Tatizo lolote linalokusumbua TUWASILIANE HAPA.

Bofya hapa
Magonjwa

MAFUA YA MISIMU (SEASONAL INFLUENZA),CHANZO NA TIBA

MAFUA YA MISIMU (SEASONAL INFLUENZA)

Huu ni ugonjwa wa ghafla na haraka wa mfumo wa upumuaji ambao husababishwa na virusi waitwao INFLUENZA. Virusi wa influenza wapo wa aina kuu tatu ambao ni influenza A, influenza B na influenza C japokua wako wa aina nyingine ambao ni hao hao aina A au B waliobadilika(mutated).

Matatizo haya hutokea kama mlipuko na huwapata watu wengi sana kwa muda mfupi,ugonjwa huu huonekana sana katika vipindi vya masika na vuli yaani vipindi vya mvua na baridi.

Mafua haya yamekua yakijitokeza karibia kila mwaka japohuwa kwa ukubwa na hali ya utofauti kidogo kidalili,na hali hii pengine huletwa na madadiliko ya virusi wenyewe. Mlipuko wa mafua unaweza kua katika nchi moja,au ukanda mmoja au dunia nzima.

ugonjwa wa mafua hua na tabia ya kusambaa sana na hivyo kama ikitokea mtu mmoja amepata ugonjwa huu basi uwezekano wa watu wengine kuambukizwa ndani ya muda mfupi ni mkubwa sana.

KWA NINI MLIPUKO WA MAFUA HUA TISHIO KWA WENGI?

Tunafahamu kwamba tunao virusi wa influenza kama influenza A,B na C,virusi hawa wamekua na tatbia ya kubadilika badilika na kuleta dalili aidha kali sana au za tofauti pale anapomuingia binadamu. Kati ya hao virusi, influenza A ndo anaonekana kuleta shida sana kwani amekua na uwezo wa kubadilika badilika sana tena kwa kiasi kikubwa kimuundo.

kwa kua influenza A ndio anaeleta sana shida ulimwenguni basi tutamjadili kidogo na namna anavyoleta matatizo kwa binadamu. Katika muktadha wa maambukizi ya influenza A viko vitu maalumu katika mwili wa kirusi huyu ambavyo kitaalamu huitwa hemagglutinin na neuraminidases ambavyo ndio kirusi wa influenza hutumia katika kuanza mashambulizi kwa binadamu.

Mpaka sasa kuna aina kadhaa ya vishambulizi hivo na muingiliano wa aina hizo ndivyo vinavyoleta majina mbalimbali ya milipuko ya mafua ,hemagglutinins zipo kama H1, H2, na H3) na neuraminidases kuna N1 na N2,mfano wa milipuko utakuta unaitwa mafua ya nguruwe ambayo kitaalamu ni H1N2.

Katika historia kumekuwepo na milipuko kadhaa ya mafua ambapo kunakuwepo na mafua makali sana na mafua ya kawaida tu. Mlipuko wa kwanza mkali wa mafua ulirekodiwa katika miaka ya 1510;

Orodha kwa ufupi ya mlipuko wa mafua ya kawaida na makali;
MLIPUKO WA MWAKA 1918-ulikua mlipuko mkali sana na ulileta maafa makubwa ikiwemo vifo vingi,mlipuko huu ulikua unafahamika kama mafua ya uhispania au mafua ya nguruwe,mafua haya yalikua yanaletwa na influenza A aina ya H1N1.

MLIPUKO WA MWAKA 1957-ulikua mlipuko mkali sana na ulileta maafa makubwa ikiwemo vifo vingi ,mafua haya yalikua yanaletwa na influenza A aina ya H2N2

MLIPUKO WA MWAKA 1968-Mlipuko huu haukua na madhara makubwa sana kwa binadamu ukilinganisha na mlipuko wa 1957, mafua haya yalikua yanaletwa na influenza A aina ya H3N2.

MLIPUKO WA MWAKA 1977-Mlipuko huu haukua na madhara makubwa sana kwa binadamu, mafua haya yalikua yanaletwa na influenza A aina ya H1N1.

MLIPUKO WA MWAKA 2009-Mlipuko huu haukua na madhara makubwa sana kwa binadamu,mafua haya yalikua yanaletwa na influenza A aina ya H1N1.

MLIPUKO WA MWAKA 2013-ulikua mlipuko mkali sana na ulileta maafa makubwa ikiwemo vifo vingi ulitokea nchini China,mlipuko huu ulifahamika kama mafua ya ndege,mafua haya yalikua yanaletwa na influenza A aina ya H7N9

Hio hapo juu ni baadhi ya milipuko katika histioria,mafua haya yameendelea kuwepo kila mwaka na yanatofautiana kidalili kutona ana eneo na eneo na aina ya kirusi huyo, kwa vipindi vyote utakua unasikia mafua ya nguruwe,ndege,mbuzi,kondoo nk lakini kirusi ni Yule Yule sema anakua amebadilika na anakua anaambukizwa kupitia wanayama tajwa kuja kwa binadamu.

TABIA ZA MILIPUKO YA MAFUA

Milipuko ya mafua hua na tabia zake,mojawapo ya tabia zake ni watu wengi kuumwa homa kali,mafua,mwili kuuma na hali hii hudumu kwa muda wa wiki 2 hadi 4 na baada ya hapo kunakua na vidalili vya kawaida ambavo huweza kukaa hadi miezi 3.

Katika hatua za awali kabisa za mlipuko wa mafua watu wanaanza kugundua kuongezeka kwa joto kali kwa watoto na mafua halafu baada ya hapo inakuja kwa watu wazima,watu wazima kuanza kua watoro kazini na wanafunzi kua watoro mashuleni.

NAMNA MAFUA YANAVYOAMBUKIZWA

Kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya mfumo wa upumuaji .njia za kuambukizwa hua ni zile zile na zinafanana.

Mafua huambikizwa kwa kuvuta hewa,matone matone madogo dogo yenye virusi hawa kutoka kwa mtu mwenye mafua, kwa maana hio ukiwa karibu na mtu mwenye mafua akiwa aidha anaongea,anapumua na we ukiwa karibu yake,anacheka,anaimba,anapiga chafya,anakohoa basi unaweza kupata maambukizi ya mafua ya influenza.

DALILI ZA MAFUA NI ZIPI?

Ugonjwa wa mafua unaweza kua wa kawaida na ukapita bila ya madhara yeyote na vile vile unaweza kua na matokeo au madhara makubwa ikiwemo kifo.

Wako baadhi ya watu wakipata mafua ya influenza wanapata homa kali sana na homa kali ya mapafu ambayo kama haitatibiwa kwa uharaka basi mtu anaweza kupoteza maisha. Ifahamike kwamba asilimia kubwa ya maambukizi haya hua ya kawaida ya yanapita,watu wachche kama wenye matatizo ya moyo,pumu,kisukari,saratani na wenye UKIMWI ndio wanaoweza kupata madhara makubwa ikiwemom kifo.

Mara tu baada ya mtu kuambukizwa kirusi wa mafua itamchukua muda wa saa 24 hadi siku mbili kuanza kupata dalili za mafua,mara baada ya mtu kupata hizi dalili ,ile siku ya kwanza na ya pili ndio mtu anakua anaumwa sana lakini siku zinazofuata mpaka siku ya 7 mtu anaanza kuona kuumwa kunapungua na mwisho anakua amepna kabisa. Zifuatazo ni dalili za mafua ya influenza

1)Homa kali(Fever)-watu wengi wanakua na joto kali,joto hucheza kati ya 37.8 hadi 41.0°C
2)Kikohozi kikavu (nonproductive cough)
3)Koo kukereketa au kuwasha au kuuma (sore throat)
4)Maumivu ya kichwa (headache)-yanaweza kua ya kawaida au makali sana
5)Kutapika na kuharisha (vomiting and diarrhea)—hii inaonekana sana sana kwa watoto kuliko watu wazima
6)Maumivu ya misuli ya mwili mzima (myalgia)
7)Kuchoka choka sana (malaise)
8)Pua kutoa maji maji au kamasi
9)Hamu ya kula kupungua au kupotea (anorexia)
10) Kizunguzungu
11) Kushindwa kupumua –hii ni mojawapo ya dalili ambayo huwapata sana watu wenye matatizo kama matatizo ya moyo,pumu,kisukari,saratani na wenye UKIMWI ambao wanapataga homa kali ya mapafu(severe pneumonia) baada ya kupata mafua.homa ya mapafu iletwayo na influenza hua ni kali na mbaya sana

MATIBABU YA MAFUA NI YAPI?

Mafua ni ugonjwa usababishwao na virusi na mara nyingi hua na dalili tajwa hapo juu lakini ni za muda mfupi na zinaisha ndani ya siku 5 au 7.

Watu wengi wamekuwa na paniki kubwa na wanakimbilia kutumia dawa za antibayotiki.

Ndugu zanguni msiwe na hofu sana juu ya mafua haya. Kwa kua mafua haya yanaisha yenyewe bila hata ya matibabu yoyote,nashauri kama mtu ukiwa na dalili za mafua uondoe hofu,ukae nyumbani angalau kwa siku 3 bila kujichanganya na wengine,hakikisha unakunywa maji mengi,punguza kuongea ongea,pumzika na tumia dawa za mafua au panado ili kuondo maumivu ya mwili na kupunguza joto.

Mara zote endapo mtu mwenye mafua akifanya hayo hupata nafuu na kupona kabisa. Pale ambapo mgonjwa anapokuja hospitali anatibiwa kulingana na hali yake alokuja nayo kwa maana kama ana joto kali basi hupewa dawa ya kuondoa joto,kama presha imeshuka au kupanda basi inatibiwa,kama sukari imeshuka atapata dripu ya kumuongezea sukari na nguvu,kama anakohoa anapata dawa za kikohozi,kama ana mafua anapata dawa za mafua na kama anapata tatizo la kupumua basi anasaidiwa ili aweze kupumua vizuri.

WITO KWA WANANCHI

Kwa kuakua kuna mlipuko wa mafua haya nawaasa mchukue tahadhari zote za kujilinda kwa kuvaa barakoa,kuepuka misongamano isiyokua ya lazima,kunywa maji mengi,kula mboga za majani na matunda kwa wingi,kuongeza matumizi ya viungo kama tangawizi,mdalasini nk.

Wananchi msipaniki kabisa juu ya mlipuko huu,ni hali ya kawaida kabisa na ukizingatia taratibu tajwa hapo juu bila shaka mafua na maudhi yake yanaisha

KWA USHAURI ZAIDI,ELIMU AU TIBA TUWASILIANE KWA NAMBA +255758286584.

Dr.Ombeni Mkumbwa

Ushauri|Tiba|CheckIn ContactUs; +255758286584 or INBOX. For More Healthtips everyday Link In http://cdp.pvh.mybluehost.me Also Follow us on Instagram @afyaclass

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.