Rais aliyeondolewa madarakani nchini Niger Mohamed Bazoum kufunguliwa mashtaka kwa makosa ya uhaini
Rais aliyeondolewa madarakani nchini Niger Mohamed Bazoum kufunguliwa mashtaka kwa makosa ya uhaini
Viongozi wa mapinduzi nchini Niger wamesema jana usiku kuwa watamfungulia mashtaka Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum kwa makosa ya uhaini wa hali ya juu na kuzorotesha usalama nchini humo.
Utawala huo wa kijeshi umesema tayari umekusanya ushahidi utakaotumika kumshitaki Bazoum pamoja na Washirika wake wa ndani na wa nje kwenye vyombo vinavyoaminika vya kitaifa na kimataifa, hii ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Kanali Meja Amadou Abdramane kupitia Televisheni ya Taifa.
Bazoumu bado anazuiliwa kwenye Kasri la Rais, pamoja na Mtoto wake wa kiume na Mkewe tangu kulipofanyika mapinduzi hayo yapata wiki ya tatu sasa.
Taarifa hiyo ya kijeshi imesema Bazoum bado anaweza kuwasiliana na Watu wa nje kwakuwa hawajazuia mawasiliano kwenye Kasri hilo la Rais na bado anakutana na Daktari wake kila wakati na hata Jumamosi hii alikutana nae na taarifa ya Daktari huyo imesema Familia yote haikuwa na tatizo lolote la kiafya, hata hivyo Rais huyo amesema anashikiliwa mateka bila ya umeme na amekuwa akilishwa wali na tambi tu.