Kwa Ushauri na Tiba Juu ya Tatizo lolote linalokusumbua TUWASILIANE HAPA.

Bofya hapa
News

Msumbiji-Niassa: Zaidi ya asilimia 40% ya wanawake hujifungua kabla ya umri wa miaka 19

#PICHA:Margarida Agida na Selma Severino, ni wauguzi waliojikita kwenye afya ya wajawazito na watoto kwenye kituo cha afya cya Lichinga, jimboni Niassa nchini Msumbiji. Hapa wanaonesha aina mbali mbali za njia za uzazi wa mpango.

Mapema asubuhi, foleni zinaanza kupangwa nje ya kituo cha afya cha Lichinga katika Jimbo la Niassa, kaskazini magharibi mwa Msumbiji, kusini mwa Afrika, huku wafanyakazi wakijiandaa kuwatibu wagonjwa. Karibu kidogo na kituo hiki, wahudumu wa afya wanatoa vipimo vya Virusi Vya Ukimwi, VVU na taarifa kuhusu mbinu za uzazi wa mpango. Hii ni hatua muhimu kwa kuzingatia jamii katika eneo hilo zinakabiliana na vurugu, ukosefu wa usalama, na mfululizo wa majanga  ya kiafya.

Mpango huo kwa mujibu wa makala iliyochipishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA nchini Msumbiji, unakaribishwa hasa na wanawake na wasichana katika mkoa wa Niassa, ambapo zaidi ya asilimia 40 ya wanawake hujifungua kabla ya umri wa miaka 19, ambapo tayari viwango vya juu vya maambukizi ya VVU ni zaidi ya mara mbili kwa wanawake, kwa asilimia 10, kuliko wanaume.

Tangu mwaka 2017, Niassa na majimbo jirani ya Cabo Delgado na Nampula yamekuwa yakikabiliwa na mashambulizi kutoka kwa makundi yasiyo ya kiserikali yaliyojihami, huku mamilioni ya watu wakikimbia makazi yao kutafuta usalama.

Hii imekuja pamoja na majanga ya mara kwa mara ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kuanzia mafuriko hadi ukame na vimbunga vikali – na dharura ya afya ya umma kama vile milipuko ya malaria na kipindupindu.

Kukosekana kwa utulivu kunaoendelea na kupungua kwa idadi ya vituo vya afya kumesababisha ujauzito na kujifungua kuwa hatari zaidi, wakati migogoro na kuhamamisha makazi kunawaweka wanawake na wasichana katika hatari kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia na biashara haramu.

Wahudumu wa afya katika kituo cha afya cha Lichinga jimboni Niassa nchini Msumbiji wamepatiwa mafunzo kuhusu mbinu za uzazi wa mpango na hutoa huduma hizo kwa jamii hata wakati wa majanga.

Kuhakikisha huduma wakati wa majanga

Licha ya majanga  yanayoendelea, zahanati ya Lichinga na kwa kushirikiana na UNFPA, Msumbiji, wamejitolea kutoa huduma muhimu za afya kwa jamii na huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

“Katika miaka mitano, huduma za afya zimebadilika, uwezo umeongezeka na uzazi wa mpango umeanza kufanya kazi, kwa msaada wa UNFPA sasa tunaweza kutoa uzazi wa mpango na njia za muda mrefu, na mimba za mapema zimepungua katika wilaya”, alisema Pascoal Vilanculos, ambaye ni kiongozi wa Idara ya Afya ya Umma huko Lichinga.

Nchini Msumbiji, ni takriban robo moja tu ya wanawake wanatumia njia za kisas aza uzazi wa mpango, na wachache zaidi katika maeneo ya vijijini, hii inatokana na ukosefu wa huduma na upatikanaji ambao umesababisha viwango vya juu vya mimba zisizotarajiwa pamoja na vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito na kujifungua pamoja na utoaji mimba usio salama.

Ili kusaidia kuziba pengo hili, UNFPA inasambaza njia za uzazi wa mpango na kuongeza uelewa kupitia timu tembezi na kliniki kote kaskazini mwa Msumbiji. Huko Niassa, watoa huduma wa afya kutoka wilaya zote 16 wamepata mafunzo juu ya njia za uzazi wa mpango za muda mrefu, kama vile vidonge vya uzazi wa mpango, vipandikizi, na vifaa vya kizazi.

Kusaidia watu wanaoishi na VVU

Kupitia kituo cha Lichinga, viongozi wa jamii na wataalamu wa kujitolea pia wamezungumza na vijana wapatao 2,500 kutoka eneo hilo, wakijadili vizuizi vya kitamaduni kuhusu afya ya ngono na unyanyapaa kuhusu VVU.

“Tunafanya hivi kwa sababu inahusu afya zetu na mustakabali wetu, na ustawi wa familia zetu, wale tunawapenda,” alieleza Filipe Jorge, mwanaharakati wa jamii ya vijana, mwenye umri wa miaka 20.

“Wakati vijana wanajipima na matokeo ni chanya, mimi hufanya nao kazi kuhusu kukubaliana na hali yao ya kujitambua, kama jamii, ni wajibu wetu kuwakaribisha.”

Mabalozi na wanaharakati wa vijana wanahimiza wengine kufanya maamuzi yaliyofikiriwa kuhusu miili yao na kuchukua jukumu la afya yao ya uzazi, pia wanashirikiana na maafisa wa afya kuhakikisha watu wanaweza kuchagua njia za uzazi wa mpango zinazokidhi mahitaji yao.

“Tunatumia hii njia shuleni kuwafanya vijana wawe na ufahamu wa uzazi wa mpango na Ukimwi, ndiyo sababu tuna kampeni ya ugawaji wa kondomu,” alielezea José Manuel, Mkurugenzi wa Huduma za Afya katika Jimbo hilo.

Wanaharakati vijana kutoka jimbo la Niassa nchini Msumbiji hupita katika vituo vya afya na shule wakijengea uwezo vijana kuhusu masuala ya afya ya uzazi.

Kukuza uhuru wa mwili

Programu za kituo cha afya ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na serikali ya Sweden katika majimbo ya Cabo Gelgado, Niassa na Nampula kwa kuzingatia na kukidhi mahitaji ya watu walio katika mazingira magumu na watu wenye ulemavu.

Ushirikiano na Radio Mocambique na redio ya kijamii ya Cuamba, au Radio Comunitaria de Cuamba pia ulitoa zaidi ya matangazo 360 ambayo yanajadili huduma za afya ya ngono, uzazi na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwasilishwa katika lugha za kienyeji kama vile kiyao, kinyanja na kimakua, na hatua hizo ziliwezesha kufikia karibu watu milioni 1.6 katika jimbo la Niassa pekee.

“Haki za kujamiiana na uzazi za wasichana zinahakikishwa, wanachagua nini cha kufanya katika miili yao, kama inavyopaswa kuwa kila mahali,” aliongeza Bw Manuel.

Dr.Ombeni Mkumbwa

Ushauri|Tiba|CheckIn ContactUs; +255758286584 or INBOX. For More Healthtips everyday Link In http://cdp.pvh.mybluehost.me Also Follow us on Instagram @afyaclass